Thu, 09 September 2010

DON BOSCO YOUTH CENTRE UPANGA

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

UTANGULIZI
Kituo cha Vijana Don Bosco upanga ni taasisi iliyochini ya Kanisa Katoliki katika Jimbo Kuu la Dar es Salaam. Kituo hiki kinaendeshwa na Wasalesiani wa Mtakatifu Don Bosco. Moja ya malengo ya kituo hiki ni kuwapa vijana fursa mbalimbali zinazoweza kuwafanya wawe Raia wema na Wakristu wazuri. Huduma zinanazotolewa kwa vijana zinagusa maeneo muhimu manne.

  1. Kimwili
    Vijana wanapata fursa mbalimbali kujikuza kimwili kupitia michezo kama mpira wa miguu, mpira wa pete, wavu, kikapu n.k
  2. Kiakili
    Vijana wanapata huduma mbalimbali za kielimu. Wanafunzi zaidi ya 200 kila siku hufika kituoni kujisomea na kujadiliana juu ya masomo yao. Pia kupitia program za kipekee kama “pre-form courses” na kwa njia ya semina na warsha maalumu kwa vipindi tofauti kadiri ya mahitaji.
  3. Kijamii
    Vijana kupitia vikundi vyao kama YCS, DB Youth4Youth, Life Choice peer educators, na klabu za michezo mfano: Karate club, Basketball club, wote kwa pamoja wanapata fursa za kupenda na kupendwa. Na hatimaye wanapokea changamoto ya kwenda nje na kuwafikia vijana wenzao kwa huduma tofauti za malezi na matendo ya huruma.
  4. Kiroho
    Kuna programs mbalimbali ili kuhakisha kuwa vijana wanapata huduma ya kiroho. Kwa vijana wa YCS wanahudumia vizuri zaidi kwa njia ya vipindi vyao vya dini mashuleni. Wanachama wa DB Youth4Youth hukutana kila jumamosi ya kwanza ya mwezi kwa malezi ya kiroho. Pia kuna programu maalumu “Misa ya Vijana na Katekesi” kila jumapili ya tatu ya mwezi. Hii ni kwa ajili ya kuwapa fursa vijana wengi zaidi kuweza kuhudumiwa kiroho.

UPEKEE WA MALEZI
Ukichunguza kwa makini utaona mpango wa malezi katika kituo cha Vijana cha Don Bosco Upanga kimehakikisha mambo manne ambayo ni nguzo muhimu sana katika kila nyumba ya Don Bosco.

  • Nyumbani – vikundi vya vijana vinakuwa familia. Kila mmoja anajisikia yupo nyumbani, ni mwanafamilia.
  • Shuleni -  kupitia huduma za kielimu wanajisikia wapo shuleni. Daima kuna mambo mapya ya kujifunza.
  • Kanisani – kwa njia ya huduma za kiroho kama katekesi, tafakari, ibada n.k vijana wanaunganika na Mungu daima.
  • Uwanjani - kwa njia ya burudani, michezo, matamasha vijana wanajisikia wamoja na urafiki hukua zaidi kati yao. Uhusiano unaongezeka, ugeni unapungua.

IDARA MBALIMBALI
WAALIMU WA DINI (CRE-TEACHERS)
Waalimu wa dini wameunganika katika makundi mawili, yaani Watawa na Walei. Idadi kubwa ya walimu ni watawa wa kike kutoka mashirika mbalimbali ya ya kitawa yaliyopo katika Jimbo kuu la Dar es salaam. Kwa sasa walimu wapo chini ya 40, wakihudumia shule za sekondari zaidi ya 90.
Bado kunachangamoto kubwa ya kupata walimu wengi zaidi ili kuweza kuwafikia wanafunzi wote.
Waalimu hufanya utume kama kundi moja. Ili kuhakikisha ufanisi wa huduma hii, gari maalumu lipo kwa ajili ya kuwahudumia waalimu waweze kufika katika shule wanazofundisha na kurudi wanakoishi.  Mratibu mkuu katika idara hii ni Pd. Fredrick Swai. Sdb

 TYCS – TANZANIA YOUNG CATHOLIC STUDENTS
Shughuli zote za YCS Jimbo la Dar es salaam zinaratibishwa na Shirika la Don Bosco kupitia kituo cha Vijana Upanga. Ofisi kuu ya Jimbo ya chama hiki ipo katika kituo cha Vijana Don Bosco-Upanga. Shughuli zote muhimu za YCS hufanyika kituoni, mfano: Ibada, Uchaguzi, Mikutano, Matamasha, Semina, Maafali, vyeti, miongozo, n.k. Hadi sasa kuna matawi zaidi ya 90 na mengine mapya yanaendelea kufunguliwa. Mlezi wa  YCS ni Pd. Fredrick Swai (Sdb), akisaidiwa na Pd. Bonifas Mchami (Sdb). 

KITUO CHA VIJANA & SYM
Kituo cha vijana (youth centre) kwa kupitia mfumo wa Salesian Youth Movement (SYM) inahudumia vikundi mbalimbali katika kituo. Vikundi vilivyopo kwa sasa ni:
DBYouth4Youth
Utume wao ni “Utume wa rika” (outreach peer ministry). Huwafikia vijana katika parokia mbalimbali za Jimbo kuu la Dar es salaam. Tayari wamekwisha toa huduma kwa parokia 20.

YCS
Ni chama cha Kitume. Kinaongozwa na vijana wenyewe na kusaidiwa na walezi. Chama kina sura ya Kimataifa. Chama kinawaidia vijana kuibua vipaji vyao kwa njia mbalimbali.

Holy Family Gospel Singers
Hiki ni kikundi cha wanafunzi kutoka shule tofauti. Pia ni wanachama wa YCS katika matawi yao. Utume wao ni kuinjilisha kwa njia ya nyimbo. Kutokana na kujisikia nyumbani wanapokua kituo cha Vijana Don Bosco - upanga, waliamua kuunda “Holy Family Gospel Singers”.

Karate Club
Club ya karate ilianzishwa mwaka 2007. Inatambulika na Shirikisho la Karate kutoka Japani. Lengo kuu: Kujitoa, Ari na stahimili ya mafunzo ni ufunguo wa ukamilifu kwa Mwanakarate. Siku za mafunzo: Jumatatu, Jumatano na Ijumaa: Watoto kuanzia saa 11:00 – 12:00 (Jioni), wakubwa kuanzia saa 12:00 – 2:00 (Jioni). Mkufunzi mkuu ni Sensei Jerome 

Savio Basketball Club
Ni moja kati ya club bora Tanzania katika mchezo wa kikapu. Katika mashindano yoyote ndani ya Tanzania huwa kati ya nafasi tatu bora. Mkufunzi mkuu ni Das.

LC-peer educators
Hawa ni watoa elimu ya kujikinga na maambukizi ya VVU/UKIMWI kwa wanarika wenzao. Kabla ya kusambaza elimu hupewa kwanza mafunzo na wanapohitimu basi huwafikia wenzao na kuwashirikisha elimu.

 

NEXT 1 | 2